Ban na Kenyatta wajadili usalama, amani na changamoto za kikanda:

Ban na Kenyatta wajadili usalama, amani na changamoto za kikanda:

Leo Jumatano Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon amekutana na Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta , na kubadilishana mawazo kuhusu masuala mbalimbali yakiwemo ya amani, usalama na changamoto za kibinadamu zinazoikabili kanda ya Afrika Mashariki.

Kuhusu uamuzi wa serikali ya Kenya kutaka kuifunga kambi ya wakimbizi ya Dadaab, Katibu Mkuu ameipongeza Kenya na watu wake kwa ukarimu waliouonyesha kwa miongo kandaa kuwapokea na kuwahifadhi maelfu ya wakimbizi kutoka mataifa mbalimbali.

Pia amemchagiza Rais Kenyatta kushirikiana na serikali ya Somalia na shirika la Umoja wa mataifa la kuhudumia wakimbizi UNHCR kwa makubaliano ya pande tatu.

Amemuhakikishia Rais Kenyatta kwamba Umoja wa mataifa utaendelea kutoa msaada wa kibinadamu, maendeleo na usalama kwa Kenya na Somalia. Ban pia ameishukuru Kenya kwa ujasiri wa vikosi vyake vilivyo sehemu ya Muungano wa Afrika AU katika kulinda amani Somalia (AMISOM) na kuelezea umuhimu wan chi hiyo kuendelea kuchangia katika vikosi vya AMISOM na juhudi zake hususani katika uchaguzi ujao mwaka huu.