Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Wahamiaji zaidi ya 60,000 wamepoteza maisha safarini tangu 1996:IOM

Wahamiaji zaidi ya 60,000 wamepoteza maisha safarini tangu 1996:IOM

Ripoti ya karibuni kabisa ya shirika la kimataifa la uhamiaji IOM iliyochapishwa leo, iitwayo "safari za kifo toleo la Pili: kuwatambua na kuwasaka wahamiaji waliokufa na kutoweka”, inasema wahamiaji zaidi ya 60,000 wanakadiriwa kufa au kupotea baharini au katika safari za nchi kavu kote duniani tangu mwaka 1996.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo takribani wahamiaji 5400 wanakadiriwa kufa au wameorodheshwa kutoweka mwaka 2015.

Na mwaka huu tayari zaidi ya wahamiaji 3400 wamepoteza maisha kote duniani wakijaribu kuingia barani Ulaya kwa njia ya bahari.

Kufuatia ripoti hiyo IOM na wadau wamekuwa na mkutano hii leo huko Berlin, Ujerumani na wadau wao kama anavyoelezea Frank Laczko, mkurugenzi wa kitengo cha uchambuzi takwimu cha IOM.

(Sauti ya Frank)

 “Sababu ya kufanya mkutano huu Berlin ni kuangalia ni hatua gani zinaweza kuchukuliwa, hususan kuangalia ni namna gani tunaweza kusaidia familia za wahamiaji waliotoweka, kuweza kufuatilia na kuwapata wapendwa wao.”