Skip to main content

Ni lazima kuripoti ukatili dhidi ya wazee kesho yaweza kuwa wewe:UM

Ni lazima kuripoti ukatili dhidi ya wazee kesho yaweza kuwa wewe:UM

Akizungumza katika kueelekea siku ya kimataifa ya kuelimisha kuhusu ukatili dhidi ya wazee, itakayoadhimishwa Juni 14, mtaalamu huru wa Umoja wa Mataifa kuhusu kufurahia haki zote za binadamu kwa wazee, Rosa Kornfeld-Matte, ameonya kwamba hakuna hatua za kutosha zinazochukuliwa kukomesha ukatili dhidi ya wazee duniani.

Bi Kornfeld-Matte ametoa wito kwa kila mtu anaeshuku ukatili dhidi ya wazee kutoa taarifa maramoja ili kuzuia kuenea kwa ukiukaji huu mkubwa wa haki za binadamu dhidi ya wazee.

Imebainika kwamba mzee mmoja kati ya 10 anakabiliwa na ukatili kila mwezi hivyo leo kwake kesho yaweza kuwa kwako ameongeza mtaalamu huyo.

Ukatili dhidi ya wazee unatokea kila mahali kwenye vituo, lakini mara nyingi majumbani na unaathiri wazee wa makundi yote, ukijumuisha ule wa kuumizwa kimwili, wa kingono, wa kifikra, kutelekezwa lakini pia wa kifedha na kunyimwa mahitaji muhimu.