Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Baraza la Usalama lalaani shambulizi la kigaidi Orlando, Florida

Baraza la Usalama lalaani shambulizi la kigaidi Orlando, Florida

Wajumbe wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, wamelaani vikali shambulizi la kigaidi lililofanyika jijini Orlando, jimbo la Florida Marekani, mnamo Juni 12 2016, ambapo watu 49 waliuawa na 53 kujeruhiwa.

Wajumbe hao wametuma risala za faraja na rambirambi kwa familia za wahanga wa shambulio hilo lililowalenga watu kwa misingi ya mwelekeo wao kimapenzi, pamoja na kwa serikali ya Marekani.

Wajumbe wa Baraza la Usalama wamekariri kuwa ugaidi wa aina zote ni moja ya matishio mabaya zaidi kwa amani na usalama wa kimataifa.

Aidha, wamekariri kuwa vitendo vyovyote vile vya kigaidi ni uhalifu na haviwezi kukubalika, bila kujali kichochezi, wakati wowote au mahala popote, au mtu yeyote yule anayevifanya.

Wamesisitiza haja ya nchi zote kukabiliana na ugaidi kwa njia zote, kulingana na Katiba ya Umoja wa Mataifa, na wajibu wao mwingine chini ya sheria ya kimataifa, ikiwemo ya haki za binadamu, sheria ya wakimbizi, na sheria ya kibinadamu.