Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Eliasson apongeza Baraza la Haki za Binadamu kwa miaka kumi ya mafanikio

Eliasson apongeza Baraza la Haki za Binadamu kwa miaka kumi ya mafanikio

Katika maadhimisho ya miaka kumi ya Baraza la Haki za Binadamu, Naibu Katibu Mkuu Jan Eliasson amesema kuundwa kwa baraza hilo kumeibua fursa kubwa ya kuongeza nguvu za mfumo wa Umoja wa Mataifa za kulinda haki za binadamu.

Akihutubia hafla iliyofanyika leo mjini Geneva Uswisi, Bwana Eliasson amemulika mafanikio yaliyopatikana katika kipindi cha miaka kumi, yakiwemo tathmini za nchi wanachama au UPR, uchunguzi wa wataalam huru wa haki za binadamu katika masuala mbali mbali zaidi, na jitihada za Baraza hilo katika kuzuia na kutatua mizozo duniani kote.

Aidha Bwana Eliasson amesisitiza kwamba bado changamoto zipo, akitaja tatizo la wakimbizi na wahamiaji, ukatili kali na katili, uhalifu wa kijinsia, ukosefu wa usawa na mzozo wa kiuchumi.

Kwa mujibu wake, suluhu ni kuhakikisha utekelezaji wa malengo ya maendeleo endelevu SDGs na kuwa na mkakati wa haki za binadamu katika masuala ya maendeleo na ulinzi wa amani, akizingatia umuhimu wa kuweka wahanga na wanaoteseka zaidi katikati ya jitihada za Umoja wa Mataifa.

Wakati huo huo, akizungumza na waandishi wa habari baada ya kuhutubia mkutano huo, Bwana Eliasson amelaani shambulizi lililofanywa dhidi ya klabu ya mashoga huko Orlando, Florida akisema tukio hilo linaibua hoja ya ulinzi dhidi ya wapenzi wa jinsia moja na wale waliobadili jinsia zao.