Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UM walaani shambulio dhidi ya raia katika swala ya Ijumaa Afghanistan

UM walaani shambulio dhidi ya raia katika swala ya Ijumaa Afghanistan

Mwakilishi maalumu wa Umoja wa mataifa nchini Afghanista Nicholas Haysom , kwa niaba ya Umoja wa mataifa amelaani vikali shambulio lililowalenga raia waliokuwa wamekusanyika kwa ajili ya swala ya Ijumaa kwenye msikiti wa Hisarak Jami wilayani Rodat, jimbo la Nangarhar nchini humo.

Shambulio hilo la leo limekatili maisha ya raia watatu na kujeruhi wengine zaidi ya 70 wakiwemo wavulana 31 huku wawili wakiwa katika hali mahtuti.

Vifaa vilivyotengwa ndani ya msikiti vimelipuka wakati wa swala ya ijumaa, na kumuua Imamu wa msikiti huo , mwanaume mwingine mmoja na mvulana waliokuwa wakisali katika Ijumaa ya kwanza ya mwezi mtukufu wa Ramadhan.

Bwana Haysom amesema shambulio la aina hiyo linalowalenga makusudi raia asilani haliwezi kuhalalishwa kwa namna yoyote ile , na linadhihirisha nia ya wahusika ya kutaka kusambaratisha maisha na kusambaza vitendo vya hofu miongoni mwa raia.

Pia ametuma salamu za rambirambi kwa familia za waliopoteza maisha na kuwatakia afueni ya haraka majeruhi.