Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mashambulizi yalenga raia Yemen: Umoja wa Mataifa walaani

Mashambulizi yalenga raia Yemen: Umoja wa Mataifa walaani

Ofisi ya Haki za binadamu imelaani mashambulizi ya roketi na makombora dhidi ya maeneo ya makazi na masoko mjini Taizz nchini Yemen yaliyotokea wiki hii na kusababisha vifo vya watu 18, wakiwemo watoto 7, na kujeruhi watu wengine 68.

Taarifa iliyotolewa leo imeeleza kwamba maeneo hayo yalikuwa yamejaa na watu wakifanya manunuzi ya kujiandaa kwa mfungo wa mwezi wa Ramadhan.

Aidha taarifa imeeleza kuwa ripoti za awali zimeonyesha kwamba mashambulizi hayo yametokea sehemu iliyotawaliwa na vikundi vilivyojihami vinavyounga mkono waHouthi na rais wa zamani Saleh.

Ofisi ya Haki za Binadamu imekumbusha kwamba raia zaidi ya 3,500 wameuawa tangu mwanzo wa mzozo mwezi Machi mwaka 2015.