Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hatma ya raia kwenye mizozo yaangaziwa na Baraza la Usalama

Hatma ya raia kwenye mizozo yaangaziwa na Baraza la Usalama

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limekutana leo kujadili kuhusu ulinzi wa raia, ambao ni msingi wa operesheni za ulinzi wa amani, kwa mujibu wa Katibu Mkuu Ban Ki-moon. Taarifa kamili na Priscilla Lecomte.

(Taarifa ya Priscilla)

Akihutubia mkutano huo ulioongozwa na Waziri wa Mambo ya Nje wa Ufaransa, Jean Marc Ayrault, Katibu Mkuu amesisitiza umuhimu wa kuwa na mkakati mzima wa kulinda raia kupitia masuala ya kijeshi, kisiasa na kiraia kwenye operesheni za ulinzi wa amani.

Hata hivyo amesema

(Sauti ya Bwana Ban)

“Lakini hata ulinzi wa amani wenye ufanisi zaidi hauwezi kulinda kila raia. Hakuna kiwango cha mkakati, rasiliamali au uwajibikaji ambacho kinaweza kupunguza madhara ya kutisha ya vita kwa wanawake, watoto na wanaume wa kawaida.”

Bwana Ban amewasihi wanachama wa Baraza hilo kuweka kipaumbele katika kutatua mizozo kupitia mikakati ya kisiasa inayoheshimu haki za binadamu

Kwa upande wake Rais wa Jamhuri ya Afrika ya Kati Faustin Archange Touadera akamulika athari za ghasia kwa raia.

(Sauti ya Rais Touadera)

“Wanawake na watoto wameathirika na uhalifu wa kingono na utumikishwaji vitani. Wakimbizi wa CAR wanataka kurudi nyumbani lakini wanataka haki, maridhiano ya kijamii na amani. Tunapaswa kwa pamoja kujitahidi zaidi kuhakikisha ulinzi wa raia kwenye nchi nzima.”