UNICEF inasaidia watoto takriban 90 walioachiliwa huru baada ya kutekwa Ethiopia
Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto UNICEF hadi leo limeshatoa msaada kwa watoto 91 wa Ethiopia, wakiwemo wasichana 45 na wavulana 46 , waliookolewa matekani baada ya majadiliano baina ya serikali ya Ethiopia na Sudan Kusini.
Watoto hawa ni sehemu ya jumla ya watoto 146 waliotekwa nyara kwenye jamii yao jimbo la Gambella Ethiopia na kupelekwa nchi jirani ya Sudan Kusini wakati wa uvamizi uliofanyika Aprili 15 mwaka huu.
Watoto hao wanapatiwa hifadhi na huduma za muda kwenye mamlaka ya serikali ya jimbo la Gambella kwa msaada mkubwa wa UNICEF.
Baadhi ya huduma wanazopata ni afya, lishe, ushauri nasaha na vifaa vingine visivyo chakula kama mahema na mavazi.
Wakati serikali ya Ethiopia na Sudan Kusini wakiimarisha juhudi zao kuokoa watoto waliosalia matekani, UNICEF wametoa wito wa kurejeshwa familia zao watoto hao, kwa usalama na bila masharti yeyote.