Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mzozo wa kisiasa Burundi waweze kuyeyusha mafanikio dhidi ya Ukimwi

Mzozo wa kisiasa Burundi waweze kuyeyusha mafanikio dhidi ya Ukimwi

Mkutano wa ngazi ya juu kuhusu Ukimwi ukiingia siku ya pili kwenye makao makuu ya Umoja wa Mataifa mjini New York, Marekani, mmoja wa washiriki kutoka Burundi amesema anatiwa hofu kuwa mzozo unaoendelea nchini humo unaweza kuwa na athari hasi kwenye mafanikio yaliyopatikana dhidi ya Virusi vya Ukimwi, VVU na Ukimwi.

Cedric Nininahazwe mwanaharakati dhidi ya Ukimwi ambaye pia alizaliwa akiwa tayari ameambukiziwa virusi hivyo, ameiambia Radio ya Umoja wa Mataifa kuwa Burundi ilikuwa kwenye mwelekeo mzuri wa kudhibiti maambukizi lakini..

(Sauti  ya Nininahazwe)

“Nina hofu kitakachokuwepo Burundi baada pengine ya mwaka mmoja, kwa sababu msisitizo wote sasa ni kwenye mzozo na nina wasiwasi kuwa tunaweza kupoteza kile tulichohangaika kwa miaka kadhaa iliyopita.”

Nininahazwe amesema mikakati ya usaidizi kwenye nchi zote zenye mizozo ikiwemo Burundi, Syria na nyinginezo isiangalie tu kumaliza mzozo bali pia kukabili kutokomeza Ukimwi na kulinda mafanikio yaliyokwishapatikana dhidi ya ugonjwa huo.