Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

MICT yaendelea kufuatilia kesi za uhalifu wa kimbari

MICT yaendelea kufuatilia kesi za uhalifu wa kimbari

Leo Baraza la Usalama limekutana kujadili operesheni za mfumo uliorithi mahakama za kimataifa za uhalifu wa Rwanda na Yugoslavia ya zamani MICT.

Rais wa MICT, jaji Theodor Meron ameripoti mafanikio ya mfumo huo katika kipindi cha miezi sita akisema maamuzi karibu 200 yamechukuliwa.

Kuhusu mahakama ya uhalifu wa Rwanda ICTR ambayo imefungwa Disemba 2015, Jaji Meron amesema utaratibu wa kukabidhi mamlaka yake kwa MICT umetimizwa vizuri, huku ujenzi wa ofisi mpya ndogo ikiwa karibu ya kukamilishwa mjini Arusha, kwa usaidizi wa serikali ya Tanzania.

Aidha amethibitisha kwamba Ladislas Ntaganzwa ambaye alikuwa amekamatwa Disemba mwaka uliopita, hivi karibuni amepelekwa Rwanda ambako kesi yake itasikilizwa.

Hatimaye Jaji Mero amekariri umuhimu wa kuendelea kusaka watoro nane waliobaki na kutimiza wajibu wa MICT kwa ajili ya wahanga na jamii zilizoathirika na uhalifu huo Rwanda na Yugoslavia ya zamani.