Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Thailand imetokomeza maambukizi ya HIV toka kwa mama kwenda kwa mtoto:UNAIDS

Thailand imetokomeza maambukizi ya HIV toka kwa mama kwenda kwa mtoto:UNAIDS

Thailand leo imepokea uthibitisho kutoka kwa shirika la afya duniani WHO kwamba imetokomeza maambukizi ya HIV na kaswende kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto, na kuwa ni taifa la kwanza barani Asia na ukanda wa Pacific , na pia nchi ya kwanza yenye idadi kubwa ya wagonjwa wa HIV kuhakikisha kuwa na kizazi huru bila ukimwi.

Waziri wa afya wa Thailand amekabidhiwa cheti cha uthibitisho kwenye hafla maalumu iliyofanyika makao makuu ya Umoja wa Mataifa New York katika mkesha wa mkutano wa baraza kuu la Umoja wa Mataifa kuhusu kutokomeza ukimwi.

Akizungumza katika hafla hiyo mkurugenzi mkuu wa UNAIDS shirika la Umoja wa mataifa la kupambana na ukimwi Michel Sidibé amesema hayo ni mfanikio makubwa sana kwa taifa ambalo maelfu ya watu wanaishi na HIV, imegeuza zahma ya ugonjwa huo na kubadfili maisha ya maelfu ya wanawake na watoto walioathirika na HIV.

Ameongeza kuwa mafanikio hayo ya Thailand yanaonyesha ni kwa kiasi gani dunia inaweza kufanikiwa wakati sayansi na dawa vinabebwa na utashi wa kisiasa.