Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Takriban miezi 6 tangu makubaliano, hali Libya bado ni tete- Kobler

Takriban miezi 6 tangu makubaliano, hali Libya bado ni tete- Kobler

Baraza la Usalama limekuwa na kikao kuhusu hali nchini Libya leo Jumatatu Juni 6, 2016, ambapo wajumbe wa Baraza hilo wamefanya mashauriano kuhusu ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Libya, UNSMIL, pamoja na vikwazo ilivyowekewa Libya.

Kikao hicho kimehutubiwa na Mwakilishi Maalum wa Katibu Mkuu, ambaye pia ni Mkuu wa UNSMIL, Martin Kobler, akisema kwamba ingawa wiki ijayo itatimu miezi sita tangu kutiwa saini makubaliano ya kisiasa nchini Libya, matumaini na matarajio waliyokuwa nayo raia wa Libya kufuatia makubaliano hayo ni kinyume kabisa na hali iliyopo sasa ya kukata tamaa.

“Utiaji saini huo ulikuwa ni mara ya kwanza kwa watu wa Libya kuamini tena kuwa inawezekana kuona amani na umoja nchini Libya. Ilikuwa mara ya kwanza kwao kuwa na matumaini kuwa bunduki zilizoleta taabu na uharibifu mkubwa maishani mwao zingenyamazishwa tena.”

Aidha, Bwana Kobler amesema utekelezaji wa makubaliano hayo umekwama, kwa sababu baadhi ya pande zilizotia saini makubaliano hayo zimeshindwa kutekeleza wajibu wao. Ametoa wito kwa bunge la wawakilishi wa kisiasa litekeleze wajibu wake wa kupiga kura ya kuridhia serikali ya umoja wa kitaifa.

“Ukizingatia ukubwa wa matatizo yanayowakabili watu wa Libya, nchi hiyo ni lazima iwe na serikali inayofanya kazi, wizara mbalimbali, na utaratibu. Hali inayozorota kasi ya haki za binadamu, hali tete ya kijeshi inayotokana na mapambano dhidi ya Daesh, inahitaji ujasiri, dhamira, na kufanya uamuzi haraka.”