Tunarejea nyumbani licha ya vitisho vya Boko Haram- UNHCR
Wakazi wa eneo la Dugwaba kwenye jimbo la Adamawa nchini Nigeria wameamua kurejea nyumbani licha ya vitisho kutoka wapiganaji wa kikundi cha kigaidi cha Boko Haram.
Miongoni mwao ni John Lukius ambaye amesema vijiji vinane kati ya 14 kwenye wilaya yao vilivyochomwa moto na wapiganaji hao mwaka mmoja uliopita lakini sasa wameona bora kurejea kwa kuwa huduma zimezidi kuzorota ugenini.
Amesema awali wenyeji waliowahifadhi huko… waliweza kuwapatia msaada lakini sasa hali inakuwa ngumu kila uchao.
Hata hivyo kurejea kwao kwa upande wa usalama kunatia matumaini kutokana na wakimbizi hao wa ndani kuamua kuunda kundi la sungusungu ambalo linafanya doria na tayari walifanikiwa kufurumusha wapiganaji wa Boko Haram.
Kwa upande wake shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi, UNHCR limesema lina wasiwasi juu ya usalama wa wakimbizi hao wa ndani huko Dugwaba, na limesihi watu hao kuahirisha kurejea kwenye maeneo yenye mapigano.