Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Leo ni siku ya mazingira duniani #WILDFORLIFE

Leo ni siku ya mazingira duniani #WILDFORLIFE

Ikiwa leo ni siku ya mazingira duniani, kila mkazi wa dunia anapaswa kuchukua hatua za kupindukia ili kulinda wanyama pori. Maadhimisho ya kimataifa yanafanyika huko Luanda, Angola kwa kutambua mchango wa nchi hiyo katika kudhibiti ujangili baada ya kupoteza idadi kubwa ya tembo kati yam waka 1975 hadi 2002.

Katika ujumbe wake wa siku hii, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon amesema maudhui ya mwaka huu yamekuja wakati muafaka kwa kuwa kuna hofu kubwa juu ya kushamiri kwa biashara haramu ya bidhaa za wanyamapori na mali za porini.

Mathalani amesema tembo wanauawa kwa sababu ya meno yao, vifaru kwa sababu ya pembe zao halikadhalika kakakuona wanauawa kwa sababu ya ngozi zao huku miti nayo ikikatwa hovyo kwa ajili ya magogo.

Ban amesema uhalifu huo unafanyika kwa ushirika baina ya vikundi vya uhalifu vilivyojipanga na makundi yenye lengo la kutikisa usalama wa nchi, hivyo ametaka siku ya leo itumike kuazimia kupinga biashara hiyo haramu akitolea mfano Angola ilivyoamua kusimama kidete kwa kupitia sheria kali kulinda mazao ya porini.

image
Maadhimisho ya siku ya mazingira duniani huko Luanda, Angola. Kutoka kulia, mwakilishi mkazi wa UM Angola, Paolo Ballodelli, Mkurugenzi mtendaji wa UNEP Achim Steiner na Waziri wa mazingira wa Angola Fatima Jardim. (Picha:UNRadio/Eleuterio Guevane)
Akizungumza katika maadhimisho mjini Luanda Angola hii leo, Mkurugenzi Mtendaji wa shirika la mazingira la Umoja wa Mataifa Achim Steiner amesema..

(Sauti ya Steiner)

“Matumaini yetu ni kwamba Angola itakuwa bingwa kubadili uchumi wake wa karne ya 20 kuwa dira ya karne ya 21 ya uchumi wa Afrika ambayo inalinda utajiri wake, inakuwa na uchumi usioharibu mazingira ambao unakwamua watu maisha, unatoa huduma za umeme, usafiri, chakula na afya bila kuharibu maliasili zake.”

Umoja wa Mataifa umeunga mkono hatua za Angola za kudhibiti ujangili kwa kusaidia katika ujenzi shule mpya ya askari wa wanyamapori kwenye jimbo la Cuando-Cubango kusini mashariki mwa nchi hiyo.

image
Mkurugenzi mtendaji wa UNEP Achim Steiner akizindua shule hiyo ya askari wa wanyamapori nchini Angola. (Picha: UNRadio/Eleuterio Guevane)
Uzinduzi ulifanyika Jumamosi na kuongozwa na Steiner ambapo amesema shule hiyo amesema itakuwa ni fursa nzuri ya kubadili majangaili kuwa walinzi wa wanyama pori.

Amesema mafunzo ni sehemu nzuri ya maendeleo na amesema inatia moyo kuona wanawake na wanaume walio tayari kupambana ili kulinda wanyama pori.

Akizungumza na Radio ya Umoja wa Mataifa huko Luanda baada ya uzinduzi huo Bwana Steiner amesema…

(Sauti ya Steiner)

“Nafikiri tumeshuhudia hatua nyingi zenye mwelekeo sahihi. Mazingira na maendeleo vinapaswa kuwa marafiki na ndugu na siyo maadui. Na ndio maana katika maadhimisho ya tarehe Tano Juni tunapoangazia biashara haramu ya bidhaa za wanyamapori, tunasherehekea uongozi wa Angola na pia hatua za waziri wa Angola za kujaribu kudhibiti na kutokomeza biashara haramu ya bidhaa za wanyamapori, lakini hii ni moja tu ya mwelekeo wa malengo endelevu.”