Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ban alaani mashambulizi ya makombora Yemen

Ban alaani mashambulizi ya makombora Yemen

Nchini Yemen, kumefanyika mashambulio kwenye mji wa Taiz, mashambulio yaliyohusisha matumizi ya silaha nzito ikiwemo roketi na makombora.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon amelaani akisema mashambulio yoyote dhidi ya maeneo ya umma ikiwemo masoko hayaruhusiwi huku akituma rambirambi kwa wafiwa na kuwatakia ahueni majeruhi.

Katika taarifa yake kupitia msemaji wake, Ban amesisitiza umuhimu wa pande zote husika kwenye mzozo kutambua kuwa kushambulia maeneo ya raia ni ukiukwaji wa sheria za kimataifa za kibinadamu na kutaka pande zote kuheshimu sheria hizo.

Pamoja na kutoa wito huo, ametaka uchunguzi huru ufanyike ili watekelezaji wa mashambulio hayo wawajibishwe.

Halikadhalika Ban ametoa wito kwa pande kwenye ambazo zinashiriki kwenye mazungumzo nchini Kuwait kuendelea kushiriki mazungumzo hayo kwa nia njema na hivyo zishirikiane na mjumbe wake Ismail Ould Cheikh Ahmed, ili kuleta amani ya kudumu na hatimaye kumaliza mzozo.

Katibu Mkuu amesema nia njema hiyo hiyo itumike kuachia huru wafungwa na wanaoshikiliwa nchini Yemen.