Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ban aomboleza kifo cha Muhammad Ali

Ban aomboleza kifo cha Muhammad Ali

Mwendazake Muhammad Ali! Mwanamasumbwi mashuhuri duniani ambaye pia alikuwa mjumbe wa amani wa Umoja wa Mataifa Muhammad Ali, amefariki dunia akiwa na umri wa miaka 74.

Hapa ilikuwa mwaka 1979 akihojiwa na waandishi wa habari kwenye makao makuu ya Umoja wa Mataifa akiulizwa masuala kadhaa kuanzia siasa hadi michezo.

Ali alikuwa ni mcheshi hata kwenye mikutano yake na waandishi wa habari alijibu maswali kwa uwazi lakini pia aliweka utani..

Nats..

 

Hapa aliulizwa swali kuhusu kesi ya wakati huo dhidi ya Zulfikar Ali Butto, aliyekuwa Waziri Mkuu wa Pakistani..

Nats..

 Ali anakiri kutofahamu akiomba radhi wanahabari huku akifarahi kuonekana kuwa ana uelewa wa mambo ambayo anaamini kuwa alipaswa kuulizwa siyo tu Rais wa Marekani bali wasomi katika nchi hiyo....

 Waandishi wa habari pia walihoji iwapo yeye ni mjumbe wa amani kulikoni anapigana masumbwi na hata wakati mwingine kuwaumiza washindani wake? Ali akizungumza na wanahabari alisema..

(Sauti ya Ali)

“Siyo kitendo ambacho huamua kama jambo ni jema au baya, bali lengo lake. Kwa nini napigana ngumi? Napigana ngumi kwa sababu ni jukwaa! Sipigani na mshindani wangu kwa kuwa eti nataka kumuumiza! Kabla ya kuanza shindano namuomba Mungu ili nisimuumize!”

 Muhammad Ali akatoa mfano..

 (Sauti ya Ali-2)

 “Jimmy Quarry nilipambama naye akaanguka chini, basi nikamwambia muamuzi asitishe pambano.  Lengo langu si kuumiza, lengo langu magazeti yaandike! Imekuwaje kijana mdogo mweusi kutoka Kentucky Kaskazini anakuja Umoja wa Mataifa na kuhutubia marais, ni kwa sababu ni mwanamasumbwi bora! Nahitaji ndondi ili nifike hapa! Kwa hiyo lengo langu ni kutumia ngumi kufikia watu.” 

image
Mwaka 1998, aliyekuwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Kofi Annan akimwekea Muhammad Ali pini yenye alama ya njiwa ambayo ni alama ya amani , baada ya kuteuliwa kuwa mjumbe wa amani wa UM. (Picha:UN/Eskinder Debebe)
Kufuatia taarifa za kifo cha Muhammad Ali, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon ametoa taarifa za masikitiko yake  huku akituma salamu za rambirambi kwa familia yake pamoja na mashabiki wake ulimwenguni kote.

Ban amesema Ali alikuwa zaidi ya mwanamasumbwi bingwa, kwani alikuwa bingwa wa usama wa na amani.

Amesema akiwa na haiba ya kusimamia misingi na ucheshi alipigania kuwepo kwa dunia yenye usawa na alitumia jukwaa la masumbwi kusaidia kutetea na kuinua ubinadamu.

Mwaka 1998 Muhammad Ali aliteuliwa mjumbe wa amani wa Umoja wa Mataifa ambalo alisafiri maeneo mbali mbali kuwatia moyo watoto na watu wengine waliokuwa wamenasa kwenye mizozo.

Hata hivyo kabla ya jukumu hilo, Ali mwaka 1978 alifika Umoja wa Mataifa kufanya kampeni ya kutokomeza ubaguzi wa rangi.

Ban anasema ilikuwa heshima kubwa kwake mwaka 2012 kuungana na Ali katika kubeba bendera ya olimpiki wakati wa mashindano ya kiangazi huko London, Uingereza.

Halikadhalika amesema kumbukumbu yake kwa mwanamasumbwi huyo ni ujasiri, ucheshi na uwezo wa kukutanisha watu pamoja.

Amehitimisha taarifa yake kwa kusema kuwa Umoja wa Mataifa unatoa shukran kubwa kwa kunufaika na maisha ya Ali walipofanya kazi pamoja karne iliyopita kusongesha ubinadamu na kutetea amani.