Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ban azingatia utashi wa kisiasa katika kufikia amani Mashariki ya Kati

Ban azingatia utashi wa kisiasa katika kufikia amani Mashariki ya Kati

Leo mjini Paris Ufaransa kumefanyika mkutano maalum kuhusu mchakato wa amani Mashariki ya Kati, uliohudhuriwa na wawakilishi wa nchi zaidi ya 30, licha ya kutokuwepo kwa wawakilishi wa Israeli na Palestina.

Akihutubia mkutano huo ulioandaliwa na serikali ya Ufaransa, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon amesema viongozi wa Palestina na Israeli wanapaswa kuchukua hatua thabiti ili kurejesha mazingira tulivu kwa mazungumzo ya amani, wakati ambapo vikwazo dhidi ya amani vimezidi.

Bwana Ban amesema vikwazo hivyo ambavyo ni pamoja na ugaidi, ghasia, uchochezi, kuenea kwa makazi ya walowezi na kukosa mshikamano kati ya Ukingo wa magharibi na ukanda wa Gaza, vinachangia katika kuhatarisha suluhu ya mataifa hayo mawili.

Amesema kinachotakiwa sasa ni utashi wa kisiasa na ujasiri wa viongozi ili kufikia makubaliano na kuyatekeleza.

Katibu Mkuu amekariri kwamba kuenea kwa makazi ya walowezi ni kinyume na sheria ya kimataifa, akiisihi jamii ya kimataifa kutumia ushawishi ili kusitisha uvamizi wa maeneo ya Palestina yaliyotawaliwa tangu 1967 na kutekeleza suluhu ya mataifa mawili.