Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UNEP-UNODC watoa taarifa kufuatia kukutwa mizoga ya watoto wa chui Thailand

UNEP-UNODC watoa taarifa kufuatia kukutwa mizoga ya watoto wa chui Thailand

Taarifa ya ugunduzi wa mizoga 70 ya watoto wa chui, na vitu vingine kama vile ngozi ya chui, hirizi na sehemu nyingine za wanyamapori kwenye hekalu la Mabuddha nchini Thailand ni mshtuko kwa watu wengi duniani kote.

Wakati mazingira ya vifo vyao bado ni kitendawili, kwa masikitiko, watoto hao wa chui ni sehemu ndogo tu ya biashara kubwa haramu ya wanyamapori ambayo inawaweka wanyama hao katika hatari ya kutoweka. Kwa mujibu wa shirika la Umoja wa Mataifa la mazingira UNEP na ofisi ya Umoja wa Mataifa ya madawa na uhalifu UNODC karibu chui 4,000 tu ndio wanaoachwa porini, na hadi biashara haramu ya wanyamapori itakaposimamishwa, kuna uwezekano mkubwa wa kuona zaidi hali ya aina hii.

Haja ya kutokomeza biashara hii haramu haraka imeufanya Umoja wa mataifa hivi karibuni kuzindua kampeni ya “Maisha kwa wanyama pori na kumtaka kila mmoja kuchukua hatua ya kukomesha usafirishaji haramu wa wanyama pori, iwe ni serikali, asasi za kiraia, makampuni ya biashara na hata watu binafsi.

Maadhimisho ya siku ya mazingira duniani hapo Juni 5 mwaka huu yanajikita  pia katika kauli mbiu ya kupambana na biashara haramu ya wanyama pori, kwa lengo la kuelimisha jamii kuhusu tatizo hilo kubwa.