Skip to main content

Ufaransa iko katika hatihati ya kukumbwa na mafuriko kama ya 1910:UNISDR

Ufaransa iko katika hatihati ya kukumbwa na mafuriko kama ya 1910:UNISDR

Maafisa mjini Paris nchini Ufaransa,  wamefunga makavazi mawili miongoni mwa makavazi maarufu zaidi duniani baada ya mto Seine kufuruka jana na kuzusha hofu ya kurudia kwa  janga la mafuriko ya mwaka 1910.

Kwa mujibu wa ofisi ya Umoja wa mataifa ya kudhibiti hatari ya majanga UNISDR, hali hiyo inaashiria umuhimu mkubwa wa maandalizi ya mipango ya kukabili majanga.

Wafanyakazi wa makavazi hayo wamekuwa wakiamisha maelfu ya kazi za Sanaa zikimwemo za Mona Lisa na kuhamishia sehemu za usalama kwa tahadhari. Miji mingi ya Mashariki na Kusini mwa mji mkuu wa Ufaransa Paris, imekabiliwa na athari kubwa za mafuriko kwa miongo kadhaa .Usafiri wa treni na pia baadhi ya barabara zimeathirika na mafuriko hayo.

Kwa mujibu wa waziri wa mazingira wa Ufaransa Bi. Ségolène Royal, asilimia 50 ya miji ya Ufaransa iko katika hatari ya mafuriko, huku watu milioni 17 kati ya watu wote milioni 67 nchini humo wanaishi katika maeneo ambayo yana hatari ya bahari, mito na mifereji kufurika.