Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Baada ya miaka miwili ya vita hali Mashariki mwa Ukraine bado mbaya: Ripoti ya UM

Baada ya miaka miwili ya vita hali Mashariki mwa Ukraine bado mbaya: Ripoti ya UM

Ripoti mpya ya ofisi ya haki za binadamu inaonyesha kwamba baada ya miaka miwili ya vita hali Mashariki mwa Ukraine inasalia kuwa tete na kuendelea kuleta athari kubwa kwa haki za binadamu, hususani kwa wale wanaoishi karibu na uwanja wa mapambano na katika maeneo yanayodhibitiwa na makundi yenye silaha.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo watu takribani 9371 wameuawa na 21,532 wamejeruhiwa Mashariki mwa Ukraine tangu kuzuka kwa mgogoro katikati ya mwezi Aprili 2014.

Ivan Simonovic, msaidizi wa Katibu Mkuu kuhusu masuala ya haki za binadamu ameonya kwamba hali ya Mashariki mwa Ukraine bado inatia hofu na bila juhudi za ziada na ubunifu wa utekelezaji wa makubaliano ya Minsk, basi inaweza kugeuka na kuwa mgogoro wa muda mrefu ambao utakuwa na madhara makubwa kwa haki za binadamu kwa miaka mingi ijayo, au machafuko yatashika kasi tena na kuongeza athari kwa watu ambao tayari wameathirika.