Umoja wa Mataifa walaani shambulio la kigaidi la Mogadishu
Baraza la Usalama limelaani shambulio lililotokea Jumatano kwenye hoteli ya Ambassador, mjini Mogadishu nchini Somalia lililosababisha vifo vya watu 15 wakiwemo wabunge wawili na majeruhi kadhaa.
Kwenye taarifa iliyotolewa leo, wanachama wa baraza hilo wametuma salamu zao za rambirambi kwa familia za wahanga pamoja na wananchi na serikali ya Somalia, wakiwatakia ahueni waliojeruhiwa.
Wakikariri kwamba ugaidi ndio tishio kubwa kwa amani ya kimataifa sasa, wanachama hao wamesisitiza umuhimu wa kupeleka watekelezaji na waandaaji wa kitendo hicho mbele ya sheria.
Aidha wamezingatia umuhimu wa kuchukua hatua ya kudhibiti ufadhili kwa kundi la Al-Shabaab na vikundi vingine vya kigaidi nchini Somalia.
Kwa upande wake Mwakilishi Maalum wa Katibu Mkuu nchini Somalia Michael Keating naye amelaani vikali shambulio hilo akisema ni la kupuuzwa, wakati ambapo wasomali wanajiandaa kwa mfungo wa mwezi mtukufu wa Ramadhan.
Bwana Keating amesema kwamba kitendo hicho kuliko kuonyesha nguvu za Al-Shabaab kinaonyesha wazi udhaifu wao na ukosefu wa maadili.