Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Nuru yaingia kwa wakazi wa Ogoni huko Nigeria

Nuru yaingia kwa wakazi wa Ogoni huko Nigeria

Serikali ya Nigeria leo imezindua mpango wa kusafisha na kurejesha katika hali ya kawaida eneo lenye mafuta la Ogoni kwenye bonde la mto Niger nchini humo.Flora Nducha na taarifa kamili.

(Taarifa ya Flora)

Mpango huo utakaogharimu dola bilioni Moja ni sehemu ya ahadi za Rais Muhammdu Buhari za kuhahikisha eneo hilo lililokumbwa na uharibifu wa mazingira kutokana na uchimbaji mafuta linarejea kwenye hali isiyokuwa na madhara kwa wakazi wake.

Akizungumza kwenye hafla ya uzinduzi wa mpango huo huko Port, Harcout, Mkurugenzi Mtendaji wa shirika la mazingira duniani, UNEP Achim Steiner amesema wakazi wa Ogoni wameathiriwa na mafanikio ya sekta ya mafuta nchini Nigeria.

Amesema hatua ya leo ni ya kihistoria ikilenga kuboresha makazi yao na hilo haliwezi kufanyika kwa siku moja bali litachukua muda likitegemea ushirikiano baina ya serikali, kampuni za mafuta na jamii zinazoishi ukanda huo wa bonde la mto Niger.

Utekelezaji wa mradi huo unazingatia ripoti yam waka 2011 ya UNEP iliyobaini madhara makubwa kwa binadamu yatokanayo na uchimbaji mafuta ikiwemo uchafuzi wa maji ya kunywa.