Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ban asikitishwa na mashambulizi dhidi ya UM Mali:

Ban asikitishwa na mashambulizi dhidi ya UM Mali:

Katibu Mkuu wa Umoja wa mataifa Ban Ki-moon amekasirishwa na mashambulizi ya kigaidi yaliyotokea jana mjini Gao Mali dhidi ya Umoja wa mataifa.

Kwa mujibu wa taarifa za awali mlinda amani mmoja kutoka China ameuawa na wengine kadhaa kujeruhiwa wakati gari lililokuwa limesheheni vifaa vya mlipuko lilipolipuka kwenye kambi ya mpango wa Umoja wa mataifa nchini Mali MINUSMA.

Na katika tukio linguine tofauti raia mmoja mjenzi kutoka Ufaransa na walinzi wawili kutoka Mali wameuawa wakati kambi ya mhandisi wa Umoja wa Mataifa katika eneo linguine la mji iliposhambuliwa na watu wasiojulikana.

Ban amesema anatiwa hofu sana na mfululizo wa mashambulizi ya karibuni dhidi ya MINUSMA ambayo yamekatili maisha ya walinda amani 12 na kujeruhi wengine wengi mwezi Mei pekee.

Ameitaka serikali ya Mali kwa msaada wa washirika wake kufanya uchunguzi haraka na kuwawajibisha wahusika. Pia ametoa wito kwa watu wa Mali kutoa taarifa za mashambulizi hayo kwa utawala.