Watoto waliokwama Falluja wanahitaji ulinzi :UNICEF

Watoto waliokwama Falluja wanahitaji ulinzi :UNICEF

Pande zote zinazopigania mji wa Fallujah nchini Iraq zinapaswa kuwalinda watoto walioko mjini humo na kutoa fursa salama ya watoto hao kuondoka limesema shirika la Umoja wa mataifa la kuhudumia watoto UNICEF.

Ghasia zinaendelea kushika kasi Fallujah wakati majeshi ya serikali yakijaribu kuukomboa mji huo kutoka mikononi mwa kundi lenye itikadi kali la Daesh au ISIL.

UNICEF inakadiria kuwa watoto takribani 20,000 bado wamekwama mjini humo ikiwa ni kilometa 60 kutoka mji mkuu Baghdad.

Kwa mujibu wa duru za habari , chakula na dawa vinakwisha na kuna upungufu wa maji safi.

Peter Hawkins mwakilishi wa UNICEF nchini Iraq anasema ni familia chache tu ndio zimefanikiwa kuondoka tangu kuanza kwa operesheni za kijeshi . Ameonya kwamba watoto wanakabiliwa na hatari ya kulazimishwa kuingizwa jeshini kupigana na kutenganishwa na familia zao.