Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UN wakaribisha mpango wa kwanza wa India kukabili majanga

UN wakaribisha mpango wa kwanza wa India kukabili majanga

Mkuu wa ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Upunguzaji hatari ya Majanga(UNISDR), Mr. Robert Glasser, leo amempongeza waziri mkuu wa India Narendra Modi, na serikali yake kwa kuanzisha mpango wa kwanza kabisa wa kitaifa kudhibiti majanga.

Bwana Glasser amesema kwa niaba ya ofisi ya Umoja wa mataifa ya kupunguza hatari ya majanga anaipongeza India kwa kuwa mfano kwa nchi zingine duniani hasa linapokuja suala la utashi wa kisiasa katika upunguzaji athari za majanga na kuzidhibiti.

Ameongeza kuwa changamoto ya upunguzaji hatari ya majanga kwa nchi kama India ni kubwa lakini taifa hilo limeonyesha kuwa penye nia pana njia na amesema amefurahi zaidi kuwa mpango huo umezingatia mkakati wa Sendai uliopitishwa na nchi wanachama wa Umoja wa mataifa.

India ni miongoni mwa nchi za kwanza duniani kujitokeza hadharani na mpango kabambe unaotaka kutekeleza vipaumbele vine vya mkakati wa Sendai, kupitia elimu na taarifa kwa umma, kuwekeza katika miundombinu inayohimili majanga, na kuboresha kiwango cha maandalizi na ujenzi mpya baada ya majanga kutokea.