Skip to main content

Guinea yatokomeza Ebola- WHO

Guinea yatokomeza Ebola- WHO

Hii leo shirika la afya duniani, WHO limetangaza kumalizika kwa maambukizi ya Ebola nchini Guinea, moja ya nchi tatu za Afrika Magharibi zilizotikiswa na ugonjwa huo.

Taarifa ya WHO imesema imechukua hatua hiyo baada ya kumalizika kwa kipindi cha siku 42 tangu mgonjwa aliyethibitika kuwa na Ebola kupimwa na kubainika hana tena virusi vya ugonjwa huo.

Kwa mantiki hiyo sasa Guinea inaingia katika kipindi cha siku 90 cha ufuatiliaji wa hali ya juu kuhakikisha visa vipya vinabainishwa mapema na kudhibitiwa kabla ya kueneza kwa watu wengine.

Christian Lindmeier ni msemaji wa WHO.

"Tutarajie masalia ya visa vingine, hilo ndilo limeelezwa awali na tumeshuhudia, visa vikiibuka. Lakini kwa kuwa nchi zimejiandaa na harakati za ufuatiliaji mashinani ziko vizuri, tuna uhakika kuwa visa vyovyote vitakavyoibuka vitashughulikiwa haraka na kwa ufanisi. Iwapo siku hizi 90 zitapia, basi maambukizi ya Ebola yatatangazwa yametokomezwa.”