Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Visa vya ugonjwa wa kuhara vyaongezeka Somalia :OCHA

Visa vya ugonjwa wa kuhara vyaongezeka Somalia :OCHA

Idadi ya visa vya ugonjwa wa kuhara imeongezeka sana mwaka huu ikilinganishwa na mwaka uliopita, imesema Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Kuratibu Misaada ya Kibinadamu OCHA ikieleza wasiwasi wake kuhusu mwelekeo huo kwenye taarifa iliyotolewa leo.

Kwa mujibu wa OCHA zaidi ya visa 7,000 vimeripotiwa katika kipindi cha miezi mitatu ya kwanza ya 2016, ikilinganishwa na visa takriban 5,000 vilivyoripotiwa kwa ujumla mwaka 2015.

OCHA imeongeza kwamba zaidi ya nusu ya waathirika ni watoto, huku vifo 300 vikiwa vimeripotiwa na shirika hilo likionya kwamba visa vingi havikuripotiwa kwa sababu maeneo yaliyoathirika hayakufikika.

Sehemu zilizoathirika zaidi ni kusini na katikati mwa Somalia.

Tayari vifurushi zaidi ya 17,000 vya kujisafi vimesambazwa, vingine 50,000 vikiwa tayari kusambazwa, huku hatua vnyingine za kinga zikichukuliwa ikiwemo mafunzo ya kuelimisha jamii na maandalizi ya mahema maalum ya kutibu kipindupindu.