Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hukumu dhidi ya Habré ni fundisho kwa wengine walio madarakani- Ban

Hukumu dhidi ya Habré ni fundisho kwa wengine walio madarakani- Ban

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon ametambua hukumu ya kifungo cha maisha iliyotolewa na mahakama maalum nchini Senegal dhidi ya Rais wa zamani wa Chad, Hissène Habré.

Stephane Dujarric ambaye ni msemaji wa Umoja wa Mataifa amemnukuu Ban akisema kuwa fikra zake zinasalia na wahanga wa vitendo vya uhalifu ambavyo vimesababisha Habré kupatikana na hatia.

Halikadhalika Katibu Mkuu amepongeza Muungano wa Afrika hususan Senegal kwa kuanzisha mahakama hiyo maalum kwa masuala ya Afrika na kutoa shukrani zake kwa nchi zote zilizowezesha utendaji kazi wake.

Amesema hukumu hiyo ni ya kihistoria na inatuma ujumbe thabiti kwa wale wote wanaotekeleza uhalifu unaotia hofu jumuiya ya kimataifa. Ikiwemo wale walioko madarakani ya kwamba watawajibika kwa vitendo wanavyofanya”.

Bwana Dujarric pia amemnukuu Kamishna Mkuu wa haki za  binadamu waUmoja wa Mataifa Zeid Ra’ad Al Hussein akizungumzia hukumu hiyo akisema..

(Sauti ya Dujarric)

 "Amepongeza makubaliano ya aina yake kati ya Senegal na Muungano wa Afrika na ambayo yaliwezesha kufanyika kwa kesi hiyo na kwamba ni mfano bora wa jinsi uongozi na umiliki wa kikanda unavyoweza kusaidia kuepusha ukwepaji wa sheria na uhalifu wa kimataifa.”

Habré, alipatikana na hatia dhidi ya mashtaka ikiwemo utumwa wa kingono, mauaji ya kukusudia, utekaji nyara watu uliofuatiwa na watu kutoweka, mateso na hata kuuawa.