Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UNAIDS: watu takribani milioni 17 wanapata dawa za HIV za kurefusha maisha

UNAIDS: watu takribani milioni 17 wanapata dawa za HIV za kurefusha maisha

Ripoti mpya ya shirika la Umoja wa mataifa linalohusika na ukimwi UNAIDS inasema idadi ya watu wanaopata dawa za kupunguza makali ya HIV imeongezeka mara mbili tangu mwaka 2010. Assumpta mMassoi na taarifa kamili..

(TAARIFA YA ASSUMPTA)

Ripoti hiyo inakadiria kwamba watu milioni 17 wamekuwa wakipata dawa hizo kufikia mwisho wa mwaka 2015, huku wengine milioni 12 wakipata fursa hivyo katika kipindi cha zaidi ya miezi 12.

Ripoti hiyo ya kimataifa ya hali ya ukimwi 2016, imetoka wakati viongozi wa dunia wakijiandaa kwa ajili ya mkutano wa baraza kuu la Umoja wa mataifa kwa ajili ya kutokomeza ukimwi utakaofanyika New York hapa Marekani kuanzia Juni 8 hadi 10 mwaka huu.

Mkuu wa UNAIDS Michel Sidibe amesema mafanikio ya dawa za kurefusha maisha yanaonekana na vifo vimepungua hasa katika nchi zilizoathirika sana katika ukanda wa Mashariki na Kusini mwa Afrika zikiwemo Kenya ,Afrika Kusini, Botswana, Eritrea, Tanzania, Malawi, Msumbiji, Uganda, Swaziland, Zambia na Zimbabwe.