Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Baraza la usalama lalaani shambulio dhidi ya walinda amani Mali

Baraza la usalama lalaani shambulio dhidi ya walinda amani Mali

Wajumbe wa baraza la usalama la Umoja wa Mataifa wamelaani vikali shambulio la kigaidi la Mei 29 dhidi ya ujumbe wa UM nchini Mali, MINUSMA katika mkoa wa Mopti ambapo walinda amani watano kutoka Togo waliuwawa.

Katika taarifa ya Baraza hilo, wajumbe wametuma salamu zao za rambirambi kwa familia za wahanga pamoja na serikali ya Togo na MINUSMA.

Wameitaka serikali ya Mali kuendesha uchunguzi dhidi ya shambulio hilo haraka na kuwafikisha watekelezaji katika vyombo vya sheria na kusisitiza kwamba shambulio dhidi ya walinda amani ni uhalifu wa kivita chini ya sheria za kimataifa.

Kadhalika baraza la usalama limekariri kuwa ugaidi, aina zake na udhihirisho wake unazidisha moja ya tishio vikubwa kwa amani na usalama wa kimataifa.