Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Stempu sita zazinduliwa kuenzi walinda amani

Stempu sita zazinduliwa kuenzi walinda amani

Ofisi ya posta ya Umoja wa Mataifa, UNPA imezindua stempu mpya sita kama sehemu ya kuenzi siku ya walinda amani duniani tarehe 29 mwezi Mei mwaka huu wa 2016.

Uzinduzi umefanyika jijini New York, Marekani wakati wa maonyesho ya dunia ya stampu ambapo mkuu wa usaidizi wa operesheni za ulinzi wa amani mashinani Atul Khare amesema ulinzi wa amani umebadilika katika miaka 65 iliyopita na kwa kushirikiana na shirika la posta la Austria wamezindua stempu kukumbuka siku hiyo adhimu.

Mbunifu wa stempu hizo Sergio Baradat amesema kupitia stempu hizo ametaka kuonyesha kiwango cha umakini wa kazi ya ulinzi wa amani na kuonyesha kile ambacho walinda amani wanafanya.

Katika stempu hizo walinda amani wake kwa waume wanaonekana wakiwa katika shughuli mbali mbali ikiwemo kutegua mabomu ya ardhini na mashauriano na raia.

Siku ya walinda amani duniani ilianzishwa na Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa mwaka 2002 na tarehe ikaridhiwa Mei 29 kwa kuwa ni siku ambayo ujumbe wa kwanza wa kusimamia amani ulianzishwa mwaka 1948 huko Palestina na Israel.