Mkutano wa LDCs wahitimishwa, waridhia benki ya teknolojia

Mkutano wa LDCs wahitimishwa, waridhia benki ya teknolojia

Mkutano wa kutathmini mpango wa utekelezaji wa Istanbul, IPoA kwa nchi zenye maendeleo duni, LDCs, umefikia ukomo hii leo huko Antalya, Uturuki ambapo miongoni mwa mambo muhimu yaliyomo kwenye nyaraka iliyopitishwa ni kuanzishwa kwa benki ya teknolojia.

Benki hiyo inalenga kusaidia nchi 48 katika sekta ya sayansi na teknolojia ambapo msaidizi wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kuhusu LDCs Gyan Acharya amesema hatua hiyo ni moja ya mafanikio makubwa ya mkutano huo wakati huu ambapo tayari Katibu Mkuu ameunda baraza simamizi la benki hiyo. Halikadhalika amesema…

"Mkutano umeibuka na masuala yenye matumaini pamoja na nyaraka yenye matarajio makubwa. Ni muhimu sana kwetu sisi kuangalia kwa kina masuala yanayohusia LDCs ili kusongesha maendeleo kwa haraka zaidi katika kipindi cha miaka mitano ijayo.”

Kwa upande wake, Naibu Katibu wa wizara ya mambo ya nje ya Uturuki, wenyeji wa mkutano huo Ayse Sinirlioglu, amesema nyaraka iliyoridhiwa inaashiria muafaka wa jamii ya kimataifa katika kusaidia nchi zenye maendeleo duni kwa kuwa..

"Imejumuisha hatua Dhahiri na mipango kama vile benki ya teknolojia kwa LDCs itakayokuwa na makazi yake Uturuki kwenye mji wa Gebze. Benki ya teknolojia itakuwa na mchango mkubwa kwa maendeleo ya sayansi na teknolojia kwa LDCS. Tunatekeleza wajibu wetu ili benki ianze kazi ifikapo mwishoni mwa mwaka huu.”