Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Tupambane na ufisadi ili kukwamua nchi za kipato duni, LDCs

Tupambane na ufisadi ili kukwamua nchi za kipato duni, LDCs

Bado jitihada zinahitajika ili kukabiliana na changamoto zinazokumba nchi zenye maendeleo duni au LDCs katika kufikia maendeleo endelevu, amesema Gyan Chandra Acharya, msaidizi wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa anayehusika na nchi hizo.

Amesema hayo akizungumza na waandishi wa habari wakati wa ufunguzi wa mkutano wa kutathmini mafanikio ya LDCs katika kutekeleza mpango kazi wao wa miaka 10 unaofanyika nchini Uturuki wiki hii. Miongoni mwa nchi 48 zilizoorodheshwa kama LDCs, 34 ziko barani Afrika.

Wakati huo huo, akihojiwa na redio ya Umoja wa Mataifa Rais wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa Mogens Lykketoft amekariri lengo la mpango kazi huo ambao ni kupunguza idadi ya nchi zenye maendeleo duni.

Bwana Lykketoft ameeleza kwamba msaada wa moja kwa moja hautatosha kuinua nchi hizo kutoka umaskini, bali amesisitizia umuhimu wa kuhakikisha kiasi kikubwa cha ukuaji wa uchumi, kupambana na ufisadi na kuimarisha mfumo wa ukusanyaji ushuru ili nchi hizo ziweze kujiendeleza.