Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ban aunga mkono Mkapa kukutana na vikundi ambavyo havikufika Arusha

Ban aunga mkono Mkapa kukutana na vikundi ambavyo havikufika Arusha

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon amekaribisha mikutano ya mazungumzo ya kisiasa nchini Burundi yaliyomalizika hivi karibuni huko Arusha, Tanzania.

Mazungumzo hayo yalifanyika chini ya uenyekiti wa Rais mstaafu wa Tanzania Benjamin Mkapa ambapo Ban amesifu uamuzi wa Mkapa wa kuitisha vikao zaidi na wadau ambao hawakuwepo Arusha.

Ban amesisitiza kuwa suluhu la kudumu la mzozo wa kisiasa nchini humo linaweza kupatiaka kupitia mchakato shirikishi ambao unazingatia katiba ya Burundi, halikadhalika misingi ya makubaliano ya Arusha kuhusu Burundi yanayodhaminiwa na Umoja wa Mataifa na ukanda wa maziwa makuu.

Katibu Mkuu kupitia msemaji wake amesema anaunga mkono juhudi za kikanda za kusaka suluhu la mzozo huo na kusisitiza utayari wa Umoja wa Mataifa kupatia usaidizi wa kiufundi na uwezeshaji kwa mujibu wa azimio la Baraza la usalama la Umoja wa Mataifa namba 2279 la mwaka 2016.