Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Vituo vya wakimbizi Ugiriki havifai kwa hifadhi ya watu- UNHCR

Vituo vya wakimbizi Ugiriki havifai kwa hifadhi ya watu- UNHCR

Shirika la Umoja wa Mataifa linalohudumia wakimbizi (UNHCR), limeeleza kusikitishwa na hali duni ya mazingira katika vituo walipohamishiwa wakimbizi na wahamiaji nchini Ugiriki, baada ya kuondolewa watu hao kwenye kambi ya muda kaskazini mwa nchi hiyo.

UNHCR imesema baadhi ya vituo vilivyotolewa na mamlaka za Ugiriki kwa hifadhi ya wakimbizi, havifai kwa makazi ya mwanadamu.

Hali hiyo pia inazua mvutano baina ya jamii mbalimbali zilizokuwa zimepewa hifadhi kwenye kambi ya Idomeni, karibu na mpaka wa Jamhuri ya zamani ya Yogoslavia ya Macedonia.

Melissa Fleming ni msemaji wa UNCHR, Geneva...

“Baadhi yao walipelekwa kwenye vituo vilivyokarabatiwa, na wengi walipelekwa kwenye mabohari na majengo ya viwanda vilivyotelekezwa, ambayo hayakuwa yameandaliwa vyema na hayakufaa kwa makazi ya mwanadamu. Kwa hiyo sasa tunahaha kufanya tuwezalo katika vituo hivyo ili angalau vifae kidogo, lakini vile tunavyodhani havifai kabisa hata ikiwa vitakarabatiwa, tunaishauri serikali iwaondoe wakimbizi hao”

Kwa mujibu wa UNHCR, baadhi ya vituo hivyo vina msongamano wa watu, na kuna uhaba wa chakula na maji, pamoja na vyoo, sehemu za kuoga na umeme.