Mabadiliko ya tabianchi yasalia mwiba ukanda wa Sahel- Chambas

Mabadiliko ya tabianchi yasalia mwiba ukanda wa Sahel- Chambas

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa leo limekuwa na kikao kuhusu changamoto za amani na usalama huko Afrika Magharibi hususan ukanda wa Sahel ambapo limeelezwa kuwa  mabadiliko ya tabianchi yamesalia tishio kwa usalama wa binadamu.

Akihutubia wajumbe kwa njia ya video kutoka Niamey, Niger, mwakilishi maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kwa Afrika Magharibi, Mohammed Ibn Chambas amesema kama hiyo haitoshi, mmonyoko wa ardhi, ongezeko la kiwango cha maji ya bahari na vitendo vya kigaidi navyo pia vinazidisha changamoto kwa nchi tano zilizo kwenye ukanda huo wa Sahel.

(Sauti ya Chambas)

“Kwa upande chanya vita dhidi ya vitendo vya kigaidi vimeanza kuleta matokeo yanayotia moyo kutokana na ushirikiano ulioimarika kati ya nchi husika na usaidizi wa dhati kutoka kwa wadau.”

Hivyo amesema kwa hatua za muda mfupi, jitihada zaidi zinahiajika ili kuunga mkono kampeni za kijeshi dhidi ya Boko haram kwenye eneo la ziwa chad ikiwemo usaidizi wa kifedha na vifaa kwa operesheni ya jeshi la pamoja, MNJTF, halikadhalika msaada kukidhi mahitaji ya kibinadamu kwa wakimbizi wa ndani ili waweze kurejea maeneo salama na hatimaye kujenga upya maisha yao.