Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Wadhamini wahimiza ushirikiano kati ya FARDC na MONUSCO uimarishwe

Wadhamini wahimiza ushirikiano kati ya FARDC na MONUSCO uimarishwe

Wawakilishi wa Wadhamini wa Mkakati wa amani, usalama na ushirikiano kwa ajili ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) wamehimiza uimarishwe ushirikiano kati ya jeshi la kitaifa la DRC, FARDC na ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini humo, MONUSCO, na kutoa wito kwa waasi wa zamani wa FDLR wakubali kurejeshwa Rwanda bila masharti.

Hayo ni kufuatia ziara ya wawakilishi hao kule Kanyabayonga (ambako watu 314 waliokuwa waasi wa FDLR wanasubiri kurejeshwa nyumbani) na Nyamilima, mashariki mwa DRC, mnamo Mei 25, 2016.

Aidha, wametumia fursa hiyo ya ziara yao kukaribisha kuanza tena operesheni za jeshi la taifa la DRC (FARDC), dhidi ya FDLR mnamo Mei 24, likisaidiwa na MONUSCO.

Hii leo, wawakilishi hao wamezuru kambi ya Munigi ya mkakati wa kujisalimisha na kurejeshwa katika jamii (DDRRR), ambako pia wamekutana na waasi wa zamani wa FDLR wanaosubiri kurejeshwa Rwanda.

Mkakati wa amani, usalama na ushirikiano kuhusu DRC unadhaminiwa na Umoja wa Mataifa, Muungano wa Afrika (AU), ICGLR na Jumuiya ya Maendeleo Afrika Kusini (SADC).