Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mwelekeo Yemen unatia matumaini- Ould Cheikh

Mwelekeo Yemen unatia matumaini- Ould Cheikh

Yemen iko katika hali tete ambapo uchumi unazidi kudorora, miundombinu imeharibiwa halikadhalika utangamano wa kijamii.

Hiyo ni kwa mujibu wa mjumbe maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kwa Yemen, Ismail Ould Cheikh Ahmed wakati akizungumza hii leo na waandishi wa habari mjini Kuwait City baada ya mazungumzo kuhusu hali ilivyo nchini Yemen.

Amesema hali si shwari lakini kuna nuru kufuatia mazungumzo ya Kuwait City akisisitiza kuwa ni suluhu la kisiasa pekee ndilo linaweza kuleta matumaini.

Bwana Ould Cheikh amesema Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon ambaye alishiriki pia mazungumzo hayo aliweka bayana kuwa ni nadra mashauriano ya amani kutokuwa na msuguano na hivyo ni lazima pande zote kwenye mzozo kuwa na stahmala.

Mjumbe huyo maalum amesema wakati wa mazungumzo hayo aliweza kuwa na mazungumzo ya kando na kila pande ambapo walijadili kwa kina jinsi ya kujumuisha kwenye makubaliano mfumo wa kujiondoa kwenye mzozo, kusalimisha silaha na kurejesha mashauriano ya kisiasa na taasisi za kitaifa.

Amesema mashauriano yataendelea na jambo la msingi ni jamii ya kimataifa kuunga mkono zaidi na kwamba Umoja wa Mataifa umeazimia kusaka suluhu la amani ya kudumu na hatimaye makubaliano thabiti yaweze kufikiwa.