Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ujumbe wa wataalam wa haki za binadamu wahitimisha zoezi la kupeleka wataalam Burundi

Ujumbe wa wataalam wa haki za binadamu wahitimisha zoezi la kupeleka wataalam Burundi

Ujumbe wa wataalam huru wa Umoja wa Mataifa walioteuliwa kuchunguza ukiukwaji wa haki za binadamu nchini Burundi, umetuma timu ya wachunguzi wa ukiukwaji huo nchini Burundi, kufuatia ziara ya ujumbe huo nchini humo mnamo mwezi Machi mwaka huu wa 2016.

Wajumbe hao waliteuliwa na Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa, kwa lengo la kutoa mapendekezo kuhusu kuboresha hali ya haki za binadamu nchini Burundi, na kuwezesha mazungumzo na mamlaka za Burundi na wadau wengine katika mgogoro wa kisiasa nchini humo.

Christof Heyns, ambaye ni mmoja wa wataalam hao huru, amesema kupelekwa kwa timu ya wataalam Burundi ni hatua muhimu katika uchunguzi wao, na kwamba kutawasaidia kukusanya taarifa kuhusu ukiukwaji wa haki za binadamu nchini humo tangu mwezi Aprili 2015.

Amesema timu hiyo haitakusanya taarifa kutoka Burundi tu, lakini pia itazuru nchi jirani za Rwanda, Uganda, Tanzania, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), ambako itakutana na wakimbizi wa Burundi na kukusanya ushahidi kutoka kwa waliokimbia ghasia.