Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mashambulizi ya Boko Haram yazorotesha hali Diffa, Niger

Mashambulizi ya Boko Haram yazorotesha hali Diffa, Niger

Shirika la Umoja wa Mataifa linalohudumia wakimbizi (UNHCR), limesema kuwa hali ya usalama na ya kibinadamu imezorota zaidi katika eneo la Diffa, kusini mashariki mwa Niger, kutokana na mashambulizi ya mara kwa mara ya Boko Haram.

Kwa mujibu wa takwimu za serikali, kufikia kati ya mwezi Mei, eneo hilo lilikuwa linawapa hifadhi watu wapatao 241,000, wakiwemo wakimbizi wa Nigeria, wakimbizi wa ndani kutoka Niger, na raia wa Niger waliokuwa wamekimbilia Nigeria.

UNHCR imesema hali ya usalama karibu na miji ya Diffa na Bosso, mashariki mwa Niger, imezorota katika miezi michache iliyopita, kutokana na vitendo vya kihalifu kila uchao, vikiwemo ulipuaji bomu wa kujitoa mhanga, katika vijiji jirani na maeneo wanayopewa hifadhi wakimbizi kutoka Nigeria na wakimbizi wa ndani.

Watu wapatao 157,000 waliokimbia vitendo vya kigaidi vya Boko Haram wanaishi katika kambi za muda karibu na mpaka wa Nigeria na Niger, na karibu na mto wa Komadougou. Kwa mujibu wa UNHCR, wengi wao walikuwa wamelazimika kuhama mara mbili au tatu kabla ya kuhamia kando ya barabara, na kwamba wanaishi kwa uoga.

Aidha, hali ya maisha ni ngumu katika mazingira hayo kame yenye joto la nyuzijoto 48 kwenye kipimo cha selsiasi, na kuna hofu ya mafuriko mvua itakapoanza kunyesha miezi miwili au mitatu ijayo