Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

WFP kuongeza bima ya majanga Afrika

WFP kuongeza bima ya majanga Afrika

Shirika la Umoja wa Mataifa la mpango wa chakula duniani WFP limesema litaongeza bima ya majanga kwa nchi nyingi zaidi barani Afrika ili kuzisaidia kuweza kukabiliana na ukame na mafuriko sio tu baada ya majanga kutokea bali pia kabla.

Hayo yamejiri wakati wa mkutano wa kusaka namna bora ya kukabiliana na majanga ya kibinadamu ulioomalizika muda mfupi  mjini Istanbul Uturuki, ambapo uwekezaji katika kushughulikia na kuhimili majanga vimeelezwa kuwa ni uwezeshaji wa kibinadamu.

WFP imetangaza kuwa ahadi ya kiasi cha zaidi ya dola milioni moja kilichotolewa na serikali ya Denmark kitatumika kusaidia sera ya bima ya uwezo wa kukabiliana na majanga barani Afrika ARC.

Gregory Barrow ni mkuu wa WFP ofisi ya London, Uingereza.

(SAUTI GREGORY)

‘‘Katika nchi nyingi za kusini mwa jangwa la Sahara, mabadiliko ya tabianchi yamesababisha maeneo mengi kuwa hatarini, sasa tunaangalia namna  tunavyoweza kiutumia bima kuweka mfumo ili yakikumbwa na ukame na wakulima wakitambua kuwa mazao yanapotea au ustawi wao uko mashakani, bima inaweza kuwapatia malipo ya fedha tasilimu.

Shirika hilo la mpango wa chakula duniani limefafanua kuwa katika kutoa bima ya majanga kwa nchi nyingi zaidi barani humo, linatarajia kupata usaidizi kutoka kwa kurugenzi ya kamisheni ya Ulaya kwa ajili ya ushirikiano wa kimataifa na maendeleo, ambayo inaunga mkono jukumu la ARC katika kujengea uwezo wa kukabiliana na ukosefu wa chakula kwa kushirikiana na serikali.