Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ban akutana na Ruto, wazungumzia Dadaab

Ban akutana na Ruto, wazungumzia Dadaab

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon ameelezea wasiwasi wake juu ya nia ya serikali ya Kenya kufunga kambi ya wakimbizi ya Dadaab kwa misingi ya usalama, uchumi na mazingira.

Akizungumza na Naibu Rais wa Kenya, William Ruto, huko Istanbul, Uturuki wanakohudhuria mkutano wa masuala ya kibinadamu, Ban amesema anatambua jukumu la kibinadamu ambalo Kenya imetekeleza kwa miaka yote lakini hatua ya kufunga kambi hiyo itakuwa na madhara kwa mamia ya maelfu ya watu.

Ban amesihi Kenya itumie fursa ya ziara ijayo ya Kamishna Mkuu wa wakimbizi Filippo Grandi nchini humo kama fursa ya kujadili zaidi suala hilo.

Kambi ya Daadab inahifadhi zaidi ya wakimbizi 300,000 na kuifanya kuwa kambi kubwa zaidi ya wakimbizi duniani.

Halikadhalika walijadili maandalizi ya uchaguzi mkuu wa Kenya mwaka 2017 ambapo Ban amesisitiza umuhimu wa mchakato wa amani wa uchaguzi na kuheshimu haki za binadamu.