UNODC na INTERPOL waazimia kuwa na ubia dhidi ya uhalifu na ugaidi
Shirika la Umoja wa Mataifa kuhusu dawa za kulevya na uhalifu (UNODC) na shirika la polisi ya kimataifa (INTERPOL), yamesaini makubaliano ya kuwa na ubia katika kupambana na chagamoto za uhalifu wa kuvuka mipaka na ugaidi.
Makubaliano hayo ya ushirikiano yamesainiwa jijini Vienna, Austria, na Mkurugenzi Mtendaji wa UNODC, Yury Fedotov na Katibu Mkuu wa INTERPOL, Juergen Stock, kandoni mwa mkutano wa 25 wa kamisheni kuhusu uhalifu.
Kupitia ushirikiano huo, mashirika hayo mawili yatabadilishana taarifa, kuimarisha ustadi wao, na kuimarisha hatua za kupambana na uhalifu wa kupangwa unaovuka mipaka na ugaidi. Akitia saini makubaliano hayo, Bwana Fedotov amesema ni dhahiri hata zaidi sasa kuwa kuna haja ya ubia wa kimataifa katika kukabiliana na changamoto za pamoja, tokean kuendeleza maendeleo endelevu, kukabiliana na tishio la uhalifu wa kupangwa unaovuka mipaka, na ugaidi.
Kazi ya mashirika hayo mawili inajumuisha kukabiliana na usafirishaji haramu wa watu na wahamiaji, ujangili wa wanyama wa pori na ulanguzi wa mali za kitamaduni. Aidha, kazi yao inahusu juhudi za pamoja dhidi ya silaha, kupambana na ufisadi na kurejesha mali zililzoibiwa, na kujenga uwezo wa kukabiliana na usafirishaji haramu wa bidhaa.