Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Fistula ni ishara ya huduma duni za afya ya uzazi- Ban

Fistula ni ishara ya huduma duni za afya ya uzazi- Ban

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-moon, amesema kuwepo ugonjwa wa fistula katika baadhi ya nchi na kanda, ni ishara ya huduma duni za afya ya uzazi katika nchi na kanda hizo.

Ban amesema hayo katika ujumbe wake wa kuadhimisha siku ya kimataifa ya fistula, akisema inamtia uchungu kuona kuwa ugonjwa huo ambao unaweza kuzuiwa na kutibiwa, bado umeshamiri duniani sasa, ukiathiri hasa wanawake na wasichana maskini zaidi, na walio hatarini zaidi, na ukiwasababishia taabu na kutengwa.

Katibu Mkuu amesema, ili kutokomeza fistula, ni lazima mifumo ya afya iimarishwe, na masuala yanayoathiri maendeleo na haki za wanawake na wasichana yashughulikiwe kwa ujumla, mathalan umaskini, usawa wa jinsia, ndoa za mapema, uzazi wa mapema na kukosa elimu.

Inakadiriwa kuwa wanawake na wasichana milioni mbili duniani wanaishi na ugonjwa wa fistula, na kuna visa vipya takriban 50,000 hadi 100,000 kila mwaka.

Ban amongeza kuwa ugonjwa wa fistula karibu umetokomezwa katika nchi zenye kipato cha juu na cha wastani, na hivyo inawezekana kuutokomeza katika kila nchi.