Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ripoti ya UNEP yamulika vifo vitokanavyo na uharibifu wa mazingira

Ripoti ya UNEP yamulika vifo vitokanavyo na uharibifu wa mazingira

Ripoti mpya ya Shirika la Mpango wa Mazingira (UNEP), imebainisha kuwa athari zitokanazo na uharibifu wa mazingira zinasababisha robo moja ya vifo vyote duniani, na hivyo kumulika haja ya kuweka suala la mazingira katika kitovu cha juhudi za kuboresha afya ya mwanadamu. Taarifa kamili na Grace Kaneiya..

(Taarifa ya Grace)

Kwa mujibu wa ripoti hiyo iliyotolewa leo wakati wa kufunguliwa kongamano la pili la Baraza la Mazingira la Umoja wa Mataifa (UNEA2), inakadiriwa kuwa kwa kila kifo kimoja kitokanacho na migogoro kila mwaka, kuna vifo 234 zaidi vitokanavyo na uharibifu na uchafuzi wa mazingira duniani.

Aidha, ripoti hiyo iitwayo “Mazingira Bora, Afya Bora” inamulika haja ya kutoa kipaumbele kwa mazingira bora, kama nguzo muhimu ya kutimiza malengo ya maendeleo endelevu.

Ripoti imesema athari za uharibifu wa mazingira zinasababisha zaidi ya robo moja ya vifo vyote vya watoto chini ya umri wa miaka mitano.