Tutunze bayonuai kwa maslahi ya sasa na baadaye- Ban

Tutunze bayonuai kwa maslahi ya sasa na baadaye- Ban

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon ametaka kuongeza juhudi za kuhifadhi bayonuai kama njia mojawapo ya kuepusha uharibifu zaidi unaoweza kuhatarisha uwepo wa sayari dunia.

Katika ujumbe wake wa kuadhimisha siku ya kimataifa ya bayonuai hii leo, Ban amesema bayonua inagusa maeneo yote ya ajenda ya maendeleo endelevu, SDGs akitaja lengo namba 15.

Lengo hilo linatambua umuhimu wa kusitisha uharibifu wa bayonuai ikiwemo mazingira ya nchi ya kavu na baharini kama njia ya kutokomeza umaskini, kupatia jamii chakula n ahata kuboresha maisha mijini.

Ban ametaja shughuli kama vile za kupanua mashamba, misitu na hata uvuvi akisema zisipotekelezwa kwa uangalifu zitaharibu bayonuai ambayo ni muhimu kwa uwepo wa vizazi vijavyo.

Kwa mantiki hiyo amesihi wadau wote wakiwemo serikali kuhifadhi kwa uendelevu viumbe hai na visivyo hai duniani akisema ni kwa maslahi ya wakazi na sayari yenyewe husika.