Skip to main content

Mwaka 2015 IOM ilisaidia wahanga 7000 wa usafirishaji haramu

Mwaka 2015 IOM ilisaidia wahanga 7000 wa usafirishaji haramu

Shirika la kimataifa la uhamiaji, IOM mwaka jana pekee liliweza kuwanasua takribani watu Elfu Saba waliokumbwa na usafirishaji haramu.

Ripoti ya IOM inasema idadi hiyo ni kubwa zaidi kuwahi kunasuliwa tangu kuanza kwa mpango wa usaidizi na ni ongezeko kwa asilimia Tisa ikilinganishwa na mwaka uliotangulia.

Mkuu wa kitengo cha usaidizi cha IOM Anh Nguyen amesema idadi kubwa ya watu hao walikuwa wanasafirishwa kiharamu ili watumikishwe kwenye kazi kama vile ujenzi, uvuvi na kazi za majumbani ilhali watu 1,400 walinasuliwa kwenye mtego wa biashara ya ngono.

Nguyen amesema IOM ina takwimu madhubuti ambazo zinaweza kusaidia watunga sera kuwa na ushahidi unaoweza kutumika katika harakati za kutokomeza usafirishaji haramu wa binadamu.