Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Watoto wakimbizi wana hatari ya kutokuwa shule mara tano zaidi ya wengine:UNESCO

Watoto wakimbizi wana hatari ya kutokuwa shule mara tano zaidi ya wengine:UNESCO

Waraka wa sera mpya uitwao “hakuna kisingizio tena”, uliotolewa kwa pamoja kwenye ripoti ya shirika la Umoja wa mataifa la elimu sayansi na utamaduni UNESCO na shirika la Umoja wa mataifa la kuhudumia wakimbizi UNHCR unasema watoto wakimbizi wako katika hatari kubwa zaidi ya kutokuwa shuleni kuliko wengine.

Ripoti hiyo iliyotoka kabla ya mkutano wa dunia wa masuala ya kibinadamu utakaofanyika Istanbul Uturuki Mei 23 na 24 inaonyesha takwimu mpya zinazoashiria kwamba asilimi 50 ya watoto wakimbizi wako katika shule za msingi na asilimi 25 vijana barubari wakimbizi ndio walio katika shule za sekondari. Nihan Koseleci ni afisa utafiti wa masuala ya elimu UNESCO

(SAUTI YA NIHAN –CUT 1)

"Tunahitaji kuwajumuisha watoto hawa na vijana barubaru kwenye mifumo ya kitaifa ya elimu, pia kuimarisha ubora wa waalimu na mafunzo kwa waalimu , ili waalimu wajiandae kukabiliana na watu wa jamii mbalimbali na watoto hawa ambao pengine hawazungumzi lugha ya nchi hiyo, au wameathirika na madhila na vita wanakotoka”

Akizungumzia umuhimu wa elimu kwa watoto hao wakimbizi mkuu wa UNESCO Irina Bokova amesema watoto hao kuwa shule wanalindwa vyema na zahma zingine nyingi kama kusafirishaji haramu wa binadamu, ndoa za utotoni, unyanyasaji wa kingono, ajira kwa watoto, na uchukuliwaji haramu wa watoto.