Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

WHO yafanya mkutano kuhusu homa ya manjano

WHO yafanya mkutano kuhusu homa ya manjano

Kamati ya dharura ya Shirika la Afya Duniani (WHO), imekuwa na mkutano kuhusu homa ya manjano kwa njia ya simu, ambao umeshirikisha nchi wanachama zilizoathiriwa na mlipuko wa homa ya manjano, zikiwa ni Angola na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC).

Sekritariati ya WHO imetoa taarifa kwa kamati hiyo kuhusu historia na ufanisi wa mkakati kuhusu homa ya manjano, mlipuko wa homa hiyo katika mji mkuu wa Angola, Luanda, pamoja na usambaaji wa homa hiyo hadi Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Uchina, na Kenya.

Kamati hiyo iliyokutana leo Alhamis Mei 19, 2016,  imepewa maelezo ya ziada kuhusu hatari ya homa ya manjano mijini barani Afrika, na hali ya akiba ya dawa ya chanjo dhidi ya homa ya manjano.

Kufuatia majadiliano kutokana na taarifa zilizotolewa, kamati hiyo imeamua kuwa homa ya manjano mijini nchini Angola na DRC, ni tukio la hatari kwa afya ya umma, ambalo linahitaji hatua za kitaifa na usaidizi wa kimataifa. Hata hivyo, kamati hiyo imeamua kuwa kulingana na maelezo yaliyopokelewa, homa hiyo siyo dharura ya afya ya umma kwa kiwango cha kimataifa.